Nafasi Ya Matangazo

April 20, 2024

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Uongozaji ndege  TCAA Bi Flora Alphonce akizungumza wakati wa mahafali.






Wahitimu wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC), kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Uganda (UCAA) wamekumbushwa kwamba kusoma hakuishii darasani pekee, mengine wataendelea kujifunza maofisini mwao  wakati wanafanya kazi husika kwa vitendo.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Uongozaji ndege  TCAA Bi Flora Alphonce aliyekuwa mgeni rasmi Aprili 19, 2024 wakati wa mahafali ya kozi za mbili za Uongozaji ndege(Area Control Procedural& Area Control Survellance). Na kuongeza kuwa anaishukuru UCAA kwa kuendelea kukiamini chuo cha CATC na kuendelea kuleta watalaam wake kwa mafunzo.

Bi Flora aliwafahamisha wahitimu hao kwamba chuo cha CATC ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo kitakuwa na majengo na vifaa vya kisasa  ambavyo vitaongeza tija na  kuleta utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazojitokeza hapa na pale kufuatia Serikali ya Tanzania kutenga Shilingi bilioni 78 kwa ajili ya mradi huo.

Awali  akizungumza  kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Chuo cha CATC Bw.Aristid Kanje alisema amefurahishwa na kuwapongeza wahitimu hao wote kwa kumaliza kozi zao kwa ufaulu wa juu. Na kuongeza kuwa ni vugumu kumlazimisha mtu kupata maarifa, kwani maarifa yanapatikana kwa kuwa na hamu ya  kuyapokea.

Wahitimu hao watano kutoka UCAA walifanya kozi mbili  kwa muda wa wiki 12, awali kabla ya mahali wahitimu hao walipatiwa semina juu ya umuhimu wa masuala ya kiafya na namna yanavyoweza kuathiri waongoza ndege katika majukumu yao kutoka kwa Daktari Concethar Mushi.

Akitoa salamu za shukran kiongozi wa darasa hilo kwa niaba ya wenzake Bw. Erasmus Muhairwe aliishukuru CATC kwa ushirikiano iliyowapatia kwa muda wote wa kozi zao na kuwakumbusha wahitimu wenzake kwamba kwa kuhitimu kwao watu wana matarajio makubwa kwao hasa ya kutokufanya makosa.
Posted by MROKI On Saturday, April 20, 2024 No comments
Mtangazaji Mahiri wa Clouds FM, Gadner G. Habash (50) amefariki Dunia Leo April 20, 2024.

Gadner maarufu kama ‘Captain’ aliejizolea Umaarufu Mkubwa kupitia Kipindi cha Jahazi, alikua amelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam kutokana na kusumbuliwa na Pressure (Shinikizo la Damu).
Marehemu Gadner amewahi pia kufanya kazi katika kituo cha Redio cha EFM na Kisha kurejea Clouds FM.
Enzi za uhali wake aliwahi kufunga ndoa na Msanii maarufu Judith Wambura a.k.a Lady Jay Dee lakini wawili hao walitengana miaka kadhaa mbele na hawakubahatika kupata mtoto. 

Marehemu ameacha mtoto na Mjukuu mmoja. 
Posted by MROKI On Saturday, April 20, 2024 No comments
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sixtus Mapunda akizungumza na timu ya wataalamu wa mazingira na ustawi wa jamii ya TARURA  na  wilaya ya Temeke



Na Mwandishi Wetu, Temeke
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sixtus Mapunda ameitaka timu ya wataalamu wa mazingira na ustawi wa jamii ya TARURA  na  wilaya ya Temeke kukaa pamoja na kutengeneza mpango kazi mzuri wa uwasilishwaji wa taarifa za utunzaji wa mazingira katika wilaya yake.

Mhe. Mapunda ameyasema hayo katika kikao cha pamoja baina yake na timu ya TARURA kilichofanyika katika ofisi yake ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya kutekeleza sheria za kutunza na kulinda mazingira kwenye mitaro ya Barabara kwa kushirikiana na wilaya zilizopo mkoa wa Dar es Salaam.

Mhe. Mapunda  ameipongeza TARURA  kwa kazi nzuri wanazofanya katika sekta ya miundombinu ya barabara wilayani Temeke na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika ulinzi wa Miundombinu hiyo. 

Timu ya wataalamu  kutoka TARURA ikiongozwa na Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mazingira na Ustawi wa Jamii Bi. Leticia Mapunda  inaendelea kufanya mazungumzo na Wakuu wa Wilaya kwa lengo la kufanya uhamasishaji  kuhusu usimamizi wa sheria ya mazingira zilizo chini ya mamlaka ya Manispaa na Jiji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Posted by MROKI On Saturday, April 20, 2024 No comments






🔴Imeshika nafasi ya Kumi kwa uzalishaji wa Kinywe Duniani

Na Mwandishi Wetu,Handeni Tanga
Mradi wa Uchimbaji na Uchenjuaji Madini ya Kinywe wa GODMWANGA GEMS LIMITED uliopo katika eneo la Kwamsisi, wilaya ya Handeni Mkoani Tanga  unatajwa kuwa mradi wa kwanza Barani Afrika kwa uchimbaji na uchenjuaji wa Madini hayo na hivyo kushika nafasi ya kumi Duniani.

Hayo yameelezwa na Meneja wa Mradi wa GODMWANGA-B  Henri Joseph wakati akizungumza na timu ya Maafisa Habari kutoka Wizara ya Madini na Wataalamu wa Tume ya Madini.

Akizungumza na timu hiyo, Joseph  amesema mradi huo umekuwa ukifanya vizuri katika uzalishaji wa madini hayo na unatarajiwa kuzalisha tani 800 kwa siku baada ya ujenzi wa kiwanda kipya kukamilika ifikapo Oktoba 2024.

Aidha, Joseph amesema mradi huo umejikita zaidi kwenye uzalishaji wa Madini Mkakati ambapo kwa sasa Dunia inauhitaji mkubwa wa madini hayo yanayotumika kutengeneza betri za magari ya umeme,  betry za simu, oil, grisi, penseli na vizuia joto.

Pia, Joseph ameeleza kuwa, Mgodi huo umefanikiwa kuigusa jamii kwa kuchangia huduma ikiwemo ujenzi wa kituo kikubwa cha Afya chenye thamani ya shilingi Milioni 200, kujenga Madarasa 6 ya shule ya Sekondari Kitumbi, kukarabati jengo la Mahakama na kukarabati barabara ya kuelekea shule ya Sekondari Kwamsisi iliyopo wilayani Handeni mkoa wa Tanga.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa GODMWANGA-A James Minja amesema Kampuni hiyo imefanikiwa kuajiri zaidi ya Wafanyakazi 200 wa kudumu na wafanyakazi 300 wa mkataba kwa lengo la kuinua vijana kiuchumi na kuendeleza uzalishaji wa Madini hayo kwa wingi.

Minja amesema kwa muda mfupi tangu kuanzishwa kwa mradi huo wamefanikiwa kupata soko kubwa la madini hayo katika nchi mbalimbali ikiwemo China na India.

Ameongeza kuwa, mpaka kufikia Oktoba mwaka 2024 kampuni hiyo itakuwa imekamilisha ujenzi unaoendelea wa mradi mkubwa zaidi ya mara kumi ya ulipo sasa ambapo inatarajiwa kuongeza uzalishaji na kupelekea Tanzania kuwa miongoni mwa nchi Tano Duniani zinazo zalisha madini ya Kinywe kwa kiwango kikubwa.

Pamoja na mambo mengine, Minja ameishukuru Serikali na kuomba kusaidiwa kuboreshewa miundombinu pamoja na huduma zingine hususan huduma za upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika.
Posted by MROKI On Saturday, April 20, 2024 No comments
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza na Timu ya mpira wa miguu ya FGA ya mkoani Ruvuma.





Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameitaka Timu ya mpira wa miguu ya FGA ya mkoani Ruvuma ambayo inashiriki Ligi Daraja la kwanza katika msimu huu wa mwaka 2023/24 iendelee kupambana na kufanya vizuri ili kucheza ligi hiyo msimu ujao.

Mhe.Ndumbaro ametoa kauli hiyo alipokutana na kuzungumza na timu hiyo Aprili 19, 2024 mjini Songea wakati timu hiyo ilipokua ikijiandaa kusafiri kwenda mkoani Mbeya kuikabili timu ya Mbeya City, Aprili 21, 2024.

Amewataka wachezaji wajiamini na kuonesha uwezo wao ili kuisaidia timu kusonga mbele pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kujiuza katika soko la ndani na nje.

Aidha, Waziri Dkt. Ndumbaro amewasisitiza wachezaji hao wapambane ili  kupata alama sita muhimu kwenye michezo miwili iliyobaki ambapo mchezo wao wa mwisho utakuwa dhidi ya Ken Gold ya Jijini Mbeya ili wajihakikishie kubaki katika nafasi nzuri katika ligi hiyo.
Posted by MROKI On Saturday, April 20, 2024 No comments

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi.





🔴Asisitiza uadilifu na uwajibikaji kwa mali za umma

Na Mwandishi wetu, Njombe
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi, amesema kazi kubwa iliyofanywa na Serikali, chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, ndani ya miaka mitatu, ni nyezo inayobeba ukweli wa kutosha kusambaratisha uongo unaoenezwa na baadhi ya wapinzani wa kisiasa kupitia mikusanyiko yao. 

Amewataka wana-CCM wote kuendelea kujiamini na kutembea kifua mbele wanapozisema, kuzitangaza na kuikumbusha jamii kuhusu kazi za maendeleo na ustawi wa jamii, zinazofanywa na Serikali za CCM ili wananchi waendelee kuuona ukweli, wakitofautisha na uongo unaoenezwa kwa propaganda nyepesi za kisiasa. 

Balozi Nchimbi amesema hayo leo, Aprili 19, 2024, alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wanaCCM wa Mkoa wa Njombe, kupitia Mkutano Maalum wa Mkoa, uliofanyika  mjini Njombe.

“Mambo yaliyofanywa na Serikali ndani ya hii miaka mitatu, unaweza kuona kama ni miujiza. Kazi kubwa sana inafanyika. Ni wajibu wetu kuitumia nyenzo yenye ukweli kupambana,” amesema.

Kupitia mkutano huo, ambao Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka aliwasilisha taarifa ya mrejesho wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 - 2025, iliyohusisha miradi mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa wananchi, Balozi Nchimbi pia amerudia kusisitiza kwa watendaji wa Chama na Serikali ulazima na umuhimu wa kuwa waadilifu wakati wote kwenye masuala yanayohusu rasilimali za umma, kwa kupiga vita rushwa na ubadhirifu.
Posted by MROKI On Saturday, April 20, 2024 No comments

April 19, 2024

Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Mradi wa Gesi Asilia wa Kampuni ya DIT Limited, Dkt. Esebi Nyari kuhusu matumizi ya gesi asilia badala ya mafuta kwenye magari alipotembelea Maonesho ya Wiki ya Nishati kwenye Viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Aprili 19, 2024
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu Nishati Safi ya Kupikia kutoka kwa Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Nishati Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage wakati wa Maonesho ya Wiki ya Nishati  Jijini Dodoma,tarehe 19 Aprili 2024.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa Maonesho ya Wiki ya Nishati Jijini Dodoma, tarehe 19 Aprili 2024.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza wakati wa Maonesho ya Wiki ya Nishati Jijini Dodoma, tarehe 19 Aprili 2024.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko  na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson baada ya kufunga Maonesho ya Wiki ya Nishati kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Aprili 19, 2024. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko baada ya kufunga Maonesho ya Wiki ya Nishati kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Aprili 19, 2024
.
*******************

🔴Ampongeza Rais Dkt. Samia kwa kutenga sh. trilioni 8.18 sekta ya nishati

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutenga fedha za kutekeleza miradi ya nishati ambapo katika kipindi cha miaka mitatu zaidi ya shilingi trilioni 8.18 zilitolewa.

 

“Maono na maelekezo yake kuhusu usimamizi wa sekta hii yamekuwa na mchango mkubwa katika ufanisi wa shughuli za sekta, katika hili, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuweka kipaumbele kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya nishati.”

 

“Katika kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa umeme nchini, tayari nchi yetu imeanza kutumia umeme wa bwawa la Julius Nyerere Hydropower Project (JNHPP). Huu ni ushindi na kielelezo tosha kwamba Mama yupo kazini.”

 

Ametoa pongezi hizo leo jioni (Ijumaa, Aprili 19, 2024) wakati akifunga Maonesho ya Wiki ya Nishati yaliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

 

Waziri Mkuu amelipongeza Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kwa kuweza kuzalisha umeme zaidi ya mahitaji yaliyopo sasa. “Leo tarehe 19 Aprili, 2024 uzalishaji wa umeme ni mkubwa. Shirika letu la TAMESCO limemudu kuzalisha umeme zaidi ya mahitaji tuliyonayo na bwawa la Julius Nyerere Hydropower Project limeanza kazi na tayari megawati 235 ziko kwenye mfumo.”

 

Ameitaka Wizara hiyo iweke mkakati wa kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa endelevu ili Waheshimiwa Wabunge waweze kupata fursa ya kuwasilisha hoja zao mahsusi na kutatua kero za wananchi wanaowawakilisha.

 

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya washiriki wa maonesho hayo ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita, Waziri Mkuu ameitaka Wizara hiyo ione uwezekano wa kuandaa maonesho kama hayo katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri. “Wakurugenzi wa Kanda na Mameneja wa Mikoa na Wilaya mko hapa. Nendeni mkae na muangalie jinsi ya kutekeleza jambo hilo,” amesisitiza.

 

Ameitaka Wizara hiyo iweke mkakati wa kuhakikisha wananchi wote wanapata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu fursa zinazopatikana kutokana na miradi inayotekelezwa na sekta ya nishati. “Pamoja na kuyaleta maonesho hapa Bungeni, kuna haja ya kupeleka maonesha kama haya kwenye maeneo ya katiati ya mji ili muweze kuwafikia wananchi wengi zaidi na kujibu hoja zao,” amesema.

 

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wadau mbalimbali walioshiriki  maonesho hayo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya umeme.

 

Naye, Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amesema sekta ya nishati ni kati ya sekta mtambuka kwa sababu inalisha sekta nyingine nyingi na ikitikisika, inatikisa na maeneo mengine pia.

 

Amesema pamoja na utoshelevu wa umeme kwenye gridi ya Taifa, ili kuwe na maendeleo bado nchi inahitaji umeme wa kutosha na hasa kwenye viwanda na siyo kuwasha taa za majumbani.

 

Ameitaka Serikali itafute njia ya kutumia vizuri maji yanayotoka kwenye bwa la JNHPP ili yaweze kuwanufaisha wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na bwawa hilo. “Bwawa limejaa kwa hiyo Serikali ihakikishe maeneo ya jirani yanapata maji ya kutumia. Tuanzishe gridi ya maji kama ilivyo kwenye gridi ya umeme. Kule chini tutengeneze njia ya kutunza maji kwa ajili ya matumizi ya umwagiliaji na mifugo,” amesema.

 

Naye, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema ushiriki wa mwaka huu umevunja rekodi kwani watu zaidi ya 480 walitembelea maonesho hayo ambapo 267 walikuwa ni Waheshimiwa Wabunge.

 

Ameyataja maeneo ambayo washiriki walikuwa wakiulizia zaidi ni umeme, nishati ya jua, nishati jadidifu, nishati safi ya kupikia, mafuta na gesi.

 

Amesema ili kujenga uelewa mpana kwa wananchi, wanapanga kuandaa kongamano maalum juu ya gesi asilia ambalo linatarjiwa kufanyika Mei, mwaka huu.

Posted by MROKI On Friday, April 19, 2024 No comments
Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego









Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego amepiga marufuku wananchi wa mkoa huo kuanza kunywa pombe asubuhi badala ya kufanya shughuli za maendeleo na za kiuchumi hali ambayo inaweza kusababisha kudumaa kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi hao na Taifa kwa ujumla.

Mkuu wa mkoa huyo ametoa kauli hiyo katika Kijiji cha Kashangu, Halmashauri ya ITIGI kwenye ziara yake ya kikazi ya Siku Mbili ya kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo ya Elimu na Afya.

HALIMA DENGEGO ameonya kuwa hatasita kuwachukulia hatua Viongozi wa Vijiji na kata ambao watashindwa kudhibiti hali hiyo ya unywaji wa pombe nyakati za asubuhi badala ya kuhimiza wananchi kwenda kufanya shughuli halali za kijitafutia riziki.

“Mnaanza kunywa Pombe asubuhi hasa watoto wa kike hii Sio sawa lazima tusimamiane nikikuta jambo linaenda ndivyo sivyo nitakamata Mtendaji kwa sababu anasheria kama zangu na kwanini ashindwe kudhibiti vitendo hivyo tutawajibishana vikali,” Amesisitiza Halima Dendego.

Kuhusu utoaji wa chakula mashuleni, Mkuu wa mkoa wa SINGIDA amewaagiza Wakuu wa Shule zote za mkoa wa SINGIDA kwa ushirikiano na Viongozi wa Vijiji na kata kuweka utaratibu wa kutoa chakula kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanajifunza kwa bidii.

Amesema utoaji wa chakula mashuleni utasaidia kwa kiasi kikubwa kupandisha ufauli kwa wanafunzi hivyo ni muhimu kwa kila shule kuanza utaratibu wa kutoa chakula kwa wanafunzi wao.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt Fatma Mganga amewataka Watendaji wa Halmashauri na Kata mkoani humo kusimamia vizuri ujenzi wa miradi ya maendeleo hasa umaliziaji wa majengo mbalimbali ili kudhibiti vitendo vya wizi wa vifaa vya ujenzi.

Amesema hatapenda kusikia wala kuona wizi wa vifaa katika miradi ya maendeleo hivyo Viongozi lazima wasimamie kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kuleta manufaa kwa Wananchi na sio vinginevyo.

Katibu Tawala huyo amesema kumekuwa na tabia kuiba vifaa hasa vinapopelekwa kwenye miradi ya maendeleo jambo ambalo linasababisha utekelezaji wa baadhi ya miradi kujengwa chini ya kiwango na kusisitiza kuwa tabia hiyo itakoma iwapo Viongozi wote watashirikiana katika ngazi zote.
Posted by MROKI On Friday, April 19, 2024 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo